Lipumba : Uchaguzi wa Rais upingwe mahakamani

0
135

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba amewasilisha mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan maeneo manne ya kipaumbele ambayo ni muhimu yakafanyiwa maboresho kwenye Katiba ya sasa kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema ni muhimu maeneo hayo yakafanyiwa maboresho kwa sababu ni wazi kuwa katiba mpya haiwezi kupatikana kabla ya mwaka 2025.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni moja, kuwezesha upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi kwa kurekebisha ibara ya 74 na kwamba tume hiyo isimamie chaguzi zote, tofauti na sasa ambapo uchaguzi wa Serikali ya Mitaa unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala.za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Eneo la pili ni katiba iruhusu mgombea binafsi kwa kufanyia maboresho ibara ya 39(2) na 67(1).

Aidha, eneo la tatu ni kufanyia maboresho ibara ya 41(6) ili itamke kuwa mshindi wa nafasi ya Urais atatangazwa endapo tu atapata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali.

Matokeo ya uchaguzi wa Rais kupingwa mahakamani ni eneo la nne ambalo TCD inapendekeza liwepo kwa kurekebisha ibara 41(7) ya katiba ya sasa.

Profesa Lipumba amesema kuwa maboresho hayo yakifanyika yatawezesha kuondoa kasoro nyingi ambazo hulalamikiwa wakati wa uchaguzi.