Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo hususani kuwawezesha Wanawake kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali katika sekta hizo.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi na Mwakilishi wa FAO upande wa Afrika, Abebe Haule-Gabriel wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.
“Naomba kutumia fursa hii kukueleza kuwa FAO tumekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania na tutaendelea kushirikiana katika kuendeleza sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuendelea kuwainua Wanawake na Vijana wanaoshiriki katika sekta hizo,” amesema Abebe.
Kwa upande wake Waziri Ulega ameishukuru FAO kwa ushirikiano wa kifedha na kitaalam inaoutoa kwaTanzania katika miradi mbalimbali inayolenga kusimamia na kuendeleza rasilimali ya uvuvi hususani utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Uvuvi Mdogo, Mpango Kabambe wa sekta ya Uvuvi na kuwawezesha Wanawake katika sekta ya uvuvi.