Tanzania Bara na Zanzibar zinatarajia kukusanya takribani Dola Milioni 2.1 kupitia mauzo ya leseni 45 za uvuvi wa bahari kuu zilizonunuliwa na wawekezaji kutoka China na Hispania.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya mauzo ya leseni hizo iliyofanyika jijini Dar-es-Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema eneo la bahari kuu upande wa Tanzania Bara na Zanzibar lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 220,000, ambazo kwa muda mrefu hazijatumika ipasavyo.
Waziri Ulega amebainisha kuwa eneo la bahari linalomilikiwa na Tanzania bara na Zanzibar lina uwezo wa kuhimili meli za uvuvi mpaka 100, na hivyo amewaomba wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu kufanya hivyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar, Suleiman Makame, amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Wizara yake, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), itasimamia na kutekeleza vipengele vyote vilivyopo kwenye leseni hizo.