BBT kunufaika na dola milioni 50

0
124

Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika umekuwa na matokeo chanya kwa upande wa program ya ‘Jenga Kesho Bora’ (BBT) kutokana na benki ya CRDB kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mazingira (GCF) kutoa kiasi cha Dola milioni 50 zitakazotumika katika utekelezaji wa program hiyo.

Hayo yamebainika wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa kuwezesha wavuvi nchini inayoratibiwa na benki ya CRDB tukio lililofanyika leo na kushuhudiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri Ulega amesema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha vijana hao wanapata mtaji mara baada ya kumaliza mafunzo yao kwa vitendo.

“Hii inamaanisha kuwa hawa wajasiriamali tunaowatengeneza kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi sasa wamepata uhakika kabisa wa kupata mikopo yao na kwa kuwa tayari wana maandiko mazuri ya biashara wataingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo mbili,” amesema Waziri Ulega.

Ulega ametoa wito kwa benki hiyo kugeukia upande wa tasnia ya ufugaji wa samaki ambako ameweka wazi kuwa anaamini kuna faida kubwa endapo wafugaji hao watawezeshwa rasilimali fedha na zana mbalimbali za kisasa za kufanyia shughuli hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, AbdulMajid Nsekela amesema mikopo yenye masharti nafuu itawapa fursa vijana hao kujipanga kwani ina muda mrefu zaidi wa matazamio kuliko aina nyingine zote za mikopo inayotolewa na benki hiyo.