Kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru Septemba 09, 2023, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na kampuni za waongoza watalii limepanga kuwapeleka Watanzania katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya kutangaza Utalii na kusherehekea siku hiyo.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara kutoka TANAPA Herman Batiho amewaambia waandishi wa Habari jijini Arusha kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru tangu ulivyopatikana mwaka 1961, lakini mwaka huu TANAPA na wadau wa Utalii wameandaa tukio hilo ili kutangaza Utalii.
Aidha, Kamishna Batiho amesema kupitia kampeni iliyopewa jina la Twenzetu Kileleni, wanatarajia kuhamasisha maelfu ya watalii wa ndani kupanda Mlima Kilimanjaro.