Dkt. Mpango: Migogoro ya ndoa imalizwe kwa amani

0
206

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Viongozi wa dini nchini kuwasaidia waumini kumaliza migogoro ya ndoa na mirathi kwa amani pasipo kuathiri watoto.

Makamu wa Rais amesema hayo aliposhiriki Ibada ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu wa nne wa Dayosisi ya Mpwawa Kanisa la Anglikana, Luzineth Kingamkono, Ibada iliofanyika wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Amesema migogoro ya ndoa na mirathi imeziathiri familia nyingi na kuwaacha akina Mama na Watoto katika madhira makubwa ikiwemo ongezeko la watoto wa mitaani, ongezeko la familia za mzazi mmoja pamoja na wajane kunyang’anywa mali walizoachiwa na wenza wao kinyume na mafundisho ya dini.

Makamu wa Rais amesema sehemu kubwa ya mmomonyoko wa maadili unaoshuhudiwa kwa sasa umechangiwa na malezi mabaya na kuvunjika kwa taasisi ya ndoa, hivyo amewahimiza wazazi na walezi nchini kutekeleza wajibu wa kuwalea Watoto na Vijana katika maadili ili kuepuka athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika familia.

Ameongeza kuwa takwimu kutoka Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonesha jumla ya talaka 442 zilisajiliwa mwaka 2019, talaka 511 zilisajiliwa mwaka 2020 na talaka 550 zilisajiliwa mwaka 2021.