Kanisa la Notre-Dame kujengwa upya

0
300

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameahidi  kulijenga upya kanisa kongwe la Katoliki la Notre-Dame lililopo jijini Paris nchini Ufaransa baada ya moto mkubwa kuteketeza kanisa hilo.

Kanisa hilo ni moja ya makanisa maarufu duniani na limekua likitembelewa na idadi kubwa ya watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani kila mwaka.

Akizungumza mara baada ya kujionea namna kanisa hilo la Katoliki la Notre-Dame lilivyoharibiwa na moto huo, Rais Macron  amesema kuwa ataitisha harambee ya Kimataifa kwa lengo la kuchangisha fedha zitakazotumika kulijenga upya kanisa hilo.

Amesema kuwa ujenzi wa kanisa hilo ni muhimu kwa kuwa lilikua ni miongoni mwa maeneo ya urithi wa Ufaransa na hata Dunia.

Habari zaidi kutoka nchini Ufaransa zinasema kuwa vikosi vya Zimamoto nchini humo vimefanikiwa kuudhibiti moto huo saa nane baada ya kuanza, na tayari ulikua umeteketeza maeneo muhimu ya kanisa hilo la kihistoria lililojengwa takribani miaka 850 iliyopita.

Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, lakini wataalamu wa ujenzi wanasema kuwa huenda ukarabati mkubwa uliokua ukiendelea kwenye kanisa hilo, ndio chanzo cha tukio hilo.

Wakati moto huo ukiendelea kuwaka, maelfu ya Raia wa Ufaransa walikusanyika katika barabara zinazoingia na kutoka katika kanisa hilo ili kushuhudia mkasa huo, huku wengine wakitokwa na machozi na wengine wakiimba nyimbo za sifa na kuomba Mungu.

Katika makanisa  mengine nchini humo, kengele zilikua zikipigwa kuashiria tukio hilo la moto.

Tayari watu mbalimbali wameanza kutoa ahadi kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo Kongwe la Katoliki la Notre-Dame akiwemo Bilionea François-Henri Pinault wa Ufaransa, ambaye ameahidi kutoa Dola Milioni 113 za Kimarekani kwa ajili ya ujenzi upya wa kanisa hilo.