Trump ajisalimisha polisi, aachiwa kwa dhamana

0
299

Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump alijisalimisha kwa Polisi katika Jimbo la Georgia kutokana na mashtaka yanayomkabili akidaiwa kujaribu kubadili matokeo ya uchaguzi kwenye jimbo hilo mwaka 2020.

Hata hivyo Trump yupo nje kwa dhamana baada ya kulipa TZS Milioni 500, ambapo sasa anasubiri kufikishwa mahakamani.

Trump ambaye anawania kugombea tena Urais wa Marekani katika uchaguzi ujao amesema kesi hiyo ni janga kwa haki, na kwamba mashitaka hayo ni ya kisiasa yanayotokana na ukweli kwamba anaonekana tishio kwa Rais Joe Biden.

Jeshi la Polisi limetoa picha ya Trump aliyopigwa baada ya kukamatwa kama inavyofanyika kwa watuhumiwa wengine ambapo namba aliyopewa ni P01135809.

Trump ameshtakiwa pamoja na watuhumiwa wengine 18 wakidaiwa walijaribu kuingilia matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo kufuatia kushindwa na mpinzani wake Joe Biden.

Alinaswa kwenye sauti ya simu akimuamuru msimamizi mkuu wa uchuguzi katika jimbo hilo kutafuta kura 11,780 wakati wa kuhesabu kura, idadi ambayo ingempa ushindi.