Parachichi ya Tanzania inayouzika zaidi nje

0
162

Mkurugenzi wa Mazao kutoka wizara ya Kilimo Nyasebwa Chimagu amesema kwa sasa Parachichi aina ya Hass na Fuerte ndio zinazouzika zaidi nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu Afrika kwa uuzaji wa parachichi.

Akizungumza na TBCOnline Chimagu amesema kwa sasa soko kubwa la parachichi lipo Ulaya, Uingereza, Uholanzi, China, Afrika ya kusini na India.

Amesema Wakulima na Wafanyabishara hawana budi kuchangamkia fursa hiyo, kwani Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jitihada kubwa kuhakikisha zao hilo linapata soko nje ya nchi hivyo wazingatie kanuni za uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.

Chimagu amebainisha kuwa kichocheo kikubwa cha wakulima kufikia viwango vya kimataifa vya uzalishaji ni uhakika wa soko la bidhaa hiyo, kwani wazalishaji watakuwa na ari ya kuzalisha kwa tija kwa kuzingatia kanuni za ubora.

Ameeleza kuwa mwelekeo wa nchi kwa sasa ni kufika kumi bora ya wazalishaji wa zao la parachichi kidunia huku pia ikiendelea na juhudi za kuongeza wigo mpana wa soko la parachichi.

Mkurugenzi huyo wa mazao kutoka wizara ya Kilimo amesema kwa sasa parachichi aina ya Hass na Fuerte ndio iliyokamata zaidi soko la nje kwa sababu ya hali yake ya uzuri wa tunda lenyewe kwa kuwa na ukubwa unaohitajika, virutubisho vya kutosha na mafuta ya kutosha.

Sifa hizo zinalifanya kuwa bora zaidi kutengeneza bidhaa za usindikaji huku ganda lake likiwa na uwezo wa kuhimili uharibifu nyakati za usafirishaji.