Benki ya Credit Suisse yaonesha imani kwa Tanzania

0
230

Benki ya Credit Suisse ya nchini Uingereza imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuipatia mkopo ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo,  baada kuridhishwa na uaminifu wa urejeshaji mikopo kwa wakati na ubora wa viwango vya miradi inayotekelezwa.

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Washington nchini Marekani na Mkurugenzi wa Masoko ya Kimataifa wa Benki hiyo Elizabeth Muchemi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango, kando ya mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha na Kimataifa.

Muchemi amesema kuwa uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya nchi zinazochukua mkopo hazitekelezi ipasavyo miradi iliyoombewa fedha,  jambo ambalo ni tofauti kwa Tanzania ambayo miradi iliyoombewa mkopo inatekelezwa vizuri na kwa viwango.

Hivi karibuni benki hiyo ya Credit Suisse ya nchini Uingereza iliipatia Tanzania mkopo wa Dola Milioni 200 za Kimarekani kwa ajili ya kutekeleza miradi mabalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya miundombinu ya barabara na reli.

“Tuko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kadri serikali itakavyoona, kwa sababu ya mipango mizuri ya serikali pamoja na kulipa madeni kwa wakati, benki ya Credit Suisse haijawahi kuwa na tatizo na Tanzania katika urejeshaji wa mikopo jambo linaloongeza imani kwa nchi hiyo”, amesema Muchemi.

Akizungumza na Mkurugenzi huyo wa Masoko ya Kimataifa wa Benki  ya Credit Suisse ya nchini Uingereza, -Elizabeth Muchemi, Waziri Mpango ameishukuru benki hiyo kwa utayari wake wa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika ugharamiaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema kuwa Tanzania imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli, barabara, umeme, maji, elimu, afya,  mradi wa gesi kimiminika, usafiri wa anga na majini, bandari, elimu, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, miradi ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa  wa rasilimali fedha.

Kwa mujibu wa Dkt Mpango, Tanzania inataka kutumia uwepo wa nchi zisizopakana na bahari kama vile Burundi, Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kujenga mtandao wa reli ya kisasa na barabara utakaosaidia kuchochea biashara na kukuza uchumi wa Taifa pamoja na ule wa nchi za Maziwa Makuu.