Rais Magufuli ahitimisha ziara katika mikoa Minne

0
517

Rais John Magufuli ameagiza kujengwa kwa kituo cha afya katika kata ya Migori mkoani Iringa ili kuondoa kero ya upatikanaji wa matibabu na akinamama wajawazito kujifungua kwa shida kwa kukosa chumba cha kujifungulia.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo waliosimamisha msafara wake akiwa njiani kuelekea jijini Dodoma.

Ameagiza kituo kicho kitakachojengwa kwa gharama ya Shilingi Milioni Mia Nne kitakapokamilika kitoe huduma za upasuaji.

Pia amewataka Wakazi wa kata hiyo ya Migori kubadilika kwa kulima mazao yanayokabiliana na ukame kutokana na kutokuwepo kwa mvua za kutosha.

Awali mbunge wa jimbo la Ismani ambaye pia ni Waziri wa Ardhi,  Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kwa niaba ya Wakazi wa jimbo hilo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaletea huduma ya maji safi na salama.

Rais amehitimisha ziara yake ya kikazi ya zaidi ya siku Kumi katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Njombe na Iringa.