Majaliwa : Watakaobainika kuiba pembejeo wachukuliwe hatua

0
158

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza watendaji wote watakaobainika kuiba pembejeo za kilimo wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wanaihujumu Serikali.

Pia amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Deogratius Mbowe amuhoji Afisa Kilimo wa Kata ya Kitama, Sharaf Manjavila kwa tuhuma za kuchukua pembejeo za Wakulima.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo mkoani Mtwara wakati akizungumza na Wananchi baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kitama wilayani Tandahimba.

Awali, baadhi ya Wananchi walimuomba Waziri Mkuu aondoke na Afisa Kilimo huyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake ikiwemo kumtuhumu kuiba pembejeo za Wakulima wa korosho.

Wakulima hao walidai kuwa walifanyiwa uhakiki na kupewa namba, ila wanapokwenda kuchukua pembejeo wanaambiwa hawajasajiliwa na majina yao hayajarudi, hivyo hawapewi dawa.

“Mashamba tulihakiki na namba tulipewa, tukifuata dawa tunaambiwa jina halijarudi na ukipeleka malalamiko yako makao makuu unaambiwa ulishachukua dawa, tatizo letu ni bwana shamba hafai.” Walisema baadhi ya Wananchi

Waziri Mkuu amewahakikishia Wananchi hao kuwa Serikali itahakikisha suala hilo linasimamiwa vizuri, hivyo waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Tandahimba kwa kushirikiana na Afisa Kilimo wa wilaya hiyo wasimamie suala la ugawaji wa pembejeo kwa Wakulma katika wilaya hiyo.