Aliyekuwa Waziri Mkuu Paskistan afungiwa siasa kwa miaka mitano

0
332

Waziri Mkuu Mstaafu wa Pakistan, Imran Khan amezuiliwa kushikilia ofisi yoyote ya umma kwa muda miaka mitano na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya rushwa, uamuzi ambao umetolewa siku tatu baada ya yeye kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Mashtaka yalihusiana na madai ya kudanganya kuhusu zawadi kutoka kwa wageni mashuhuri wa kigeni na mapato yaliyotokana na mauzo ya zawadi hizo ambazo ni saa za Rolex, pete na vifungo ambavyo kwa pamoja vimeripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5.

Imran Khan, ambaye aliteuliwa kuwa kiongozi wa Pakistan mwaka 2018 na kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye mwaka 2022 baada ya kuwa na mzozo na jeshi nchini humo amesema kuwa, mashtaka dhidi yake ni ya kisiasa, lakini serikali inakanusha hilo na inasisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa mujibu wa sheria.

Kufuatia uamuzi huo, Imran Khan pia atafutwa Ubunge.

Sheria za Pakistan zinakataza mtu aliyehukumiwa kuwania uongozi wa ofisi za umma kwa kipindi maalum kilichowekwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Timu yake ya kisheria imepinga hukumu hiyo na kesi itasikilizwa katika Mahakama Kuu ya Islamabad.