Wizara ya Maji yatakiwa kusimamia miradi kikamilifu

0
581

Rais  John Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha Shilingi Bilioni 45 zilizotolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji katika mji wa  Makambako mkoanji Njombe,  zitatumika kama ilivyokusudiwa.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo mkoani Njombe  mara baada ya kufungua barabara ya Mafinga – Nyigo – Igawa yenye urefu wa kilomita 138.7 katika eneo la Mtewele  mjini Makambako, barabara itakayotumiwa pia na nchi za  Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Amesema kuwa  amelazimika kutoa agizo kutokana na ushahidi kuonyesha kuwa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maji zimekua zikipotea kwa kutekeleza miradi hewa.

Rais Magufuli ametolea mfano kipindi cha mwaka 2013 hadi mwaka 2018 ambapo ulifanyika uhakiki wa miradi ya maji yenye thamani ya Shilingi Bilioni 119 ambapo miradi ya ukweli ilikua ni ya Shilingi Bilioni 17 pekee na mingine ilikua hewa.

Halkadhalika amewapongeza wakazi wa mkoa wa Njombe kuwa wachapakazi, hali iliyochangia mkoa huo kuwa na maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya kilimo.

Rais Magufuli amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku Tatu mkoani Njombe na anatarajiwa kuanza ziara yake mkoani Iringa.