Mbao FC wapanda kileleni mwa Ligi Kuu

0
2300

Wabishi wa Mwanza, Mbao FC wamepanda kileleni mwa ligi kuu Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa ugegeni wa bao mbili kwa moja dhidi ya Stand United – Chama la Wana ya Shinyanga.

Pamoja na Stand United kutangulia kupata goli kwenye dakika ya 31 kupitia kwa Sixtus Sabela lakini walishindwa kulinda goli hilo na Mbao FC kufunga magoli hayo mawili kupitia kwa Said Hamis kwenye dakika ya 54 na Pastory Athanas akapigilia goli la ushindi kwenye dakika ya 59.

Huo ni ushindi wa pili wa Mbao FC tangu kuanza kwa msimu wa ligi kuu baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa bila kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya wapinzani wao wa mji mmoja Alliance FC .

Nao mabingwa wa kombe la Shirikisho Mtibwa Sugar wamepata ushindi wao wa kwanza kwenye ligi kuu msimu huu baada ya kuifunga timu ngumu ya Tanzania Prisons bao moja kwa bila, bao lililofungwa kwenye dakika ya 37 na mshambuliaji wa kati Stamili Mbonde.

Katika michezo mingine Ruvu Shooting, – wazee wa kupapasa wamebanwa mbavu na kutoka sare ya bao moja kwa moja na timu mpya ya KMC, huku Wanapaluhengo Lipuli FC wakiendeleza sare baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na JKT Tanzania.