Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo amesema bidhaa nyingi za sekta ya kilimo zinazoingizwa au kutolewa nchini za sekta hiyo zina misamaha ya kodi.
Kayombo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Mbeya, akisisitiza Wananchi kujiingiza katika kilimo kutokana na fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
Amesema kuwa msamaha huo unahusisha hata pale mkulima anapouza bidhaa nje ya nchi kwa kuwa hatozwi kodi ya aina yoyote ile isipokuwa kwa bidhaa ya korosho na ngozi ghafi.
Kayombo ameongeza kuwa bidhaa hizo sio tu kwa zile ambazo hazijaongezwa thamani bali hata kwa zilizoongezwa thamani pia zote zina misamaha ya kodi pale zinapopelekwa nje ya nchi.
Kayombo ameujulisha umma kuwa kwa sasa kodi ya uagizaji wa vitenge nchini imepunguzwa kutoka asilimia 50 hadi 35, huku ile namna ya ukadiriaji kodi za vitenge hivyo nayo ikiwa imefanyiwa marekebisho kwa kuweka unafuu wa ulipaji wa kodi hiyo ili kutokomeza magendo ya vitenge ndani ya nchi.