Urusi wanataka kuleta ndege Tanzania

0
172

Waziri Mkuu kassim Majaliwa amesema Urusi inataka kuleta ndege zitakazofanya safari zake kutoka nchini humo hadi Tanzania, ambapo kwa sasa nchi hiyo inakamilisha taratibu za makubaliano na Serikali ya Tanzania.

Akikagua mabanda ya maonesho ya Sherehe ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane mkoani Mbeya, Waziri Mkuu Majaliwa amesema makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha kuna usalama wa ndege za Urusi na Wafanyakazi wake, hivyo zikikamilika ndege hizo zitaanza safari zake nchini Tanzania.

Waziri mkuu ameongeza kuwa kwa historia katika kipindi cha miaka kumi iliyopita wakati ndege za Urusi zilipokuwa zikija Tanzania idadi ya watalii iliwahi kufika elfu 72 kutoka Urusi peke yake ndani ya mwaka mmoja.

Amesema kwa sasa kuna haja ya kurudisha watalii hao, na hivyo kuliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwenda mbali zaidi kimipango ili kujiandaa na mapokezi ya watalii hao kutoka Urusi.