Uchunguzi wabaini madudu sakata la mkimbiaji wa Somalia

0
217

Serikali ya Somali imemsimamisha kazi afisa michezo kwa upendeleo baada ya kumpelekea ‘mwanamichezo’ asiye na sifa kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

Nasra Abukar Ali alitumia takribani sekunde 22 kukimbia mita 100, ikiaminika kuwa ni muda mrefu zaidi kuwahi kutumika kwenye kipengele hicho, ambapo anashiriki mashindano ya vyuo vikuu nchini China.

Uchunguzi uliofanywa na Wizara ya Michezo na Vijana ya Somalia umeonesha kuwa Nasra si mkimbiaji na si mwanamichezo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo Somalia, Khadijo Aden Dahir ametuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake na kuiaibisha nchi, ambapo sasa amesimamishwa kazi.

Aidha, uchunguzi wa wizara umebaini pia kuwa, kile kinachoitwa Shirikisho la Michezo la Vyuo Vikuu Somalia hakipo, na kuahidi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote waliohusika.

Licha ya uwepo wa tuhuma za upendeleo, wizara haikueleza uhusiano uliopo kati ya Nasra na Khadijo.