Hatma ya golikipa wa Simba kujulikana leo

0
452

Afisa Habari Simba SC, Ahmed Ally amesema ripoti ya daktari itakayotolewa leo juu ya majeraha ya golikipa waliyemsajili karibuni kutoka Brazil, Jefferson Luis itaamua kama wataendelea naye au wataingia sokoni kutafuta golikipa mwingine.

Ally amesema Luis ameumia akiwa mazoezini nchini Uturuki na kwamba ripoti ikionesha majeraha yatamchukua muda mrefu kupona, Simba pasi na shaka itaachana naye na kutafuta mchezaji mwingine wa kuziba nafasi hiyo.

“Kama itaonekana anaweza kupona ndani ya siku mbili, siku tatu, tutaendelea naye,” amesema huku akiongeza kuwa, ripoti hiyo ikionesha kuwa majeraha yamepoa kwa muda, kwamba kuna uwezekano akaumia mbeleni, hawataendelea naye kwani wanataka apone kabisa.

Ameongeza kuwa klabu hiyo imelazimika kutafuta kipa mpya kutokana na Aishi Manula kubainika kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa miezi minne akiuguza jeraha alilopata mwishoni mwa msimu.

Luis alikuwa ameletwa kuongeza nguvu kwenye safu ya magolikipa wa Simba akiungana pamoja na Ahmad Feruz na Ally Salim.