Wanaume wanaofanyiwa ukatili watakiwa kupaza sauti

0
172

Wanaume wanaofanyiwa ukatili katika familia zao wametakiwa kuacha utamaduni wa kunyamaza kimya wakiogopa kuchekwa ama kujidhalilisha, kwani kufanya hivyo huchangia kutokwisha kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi yao.

Hayo yamefahamika wakati wa kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria ikiendelea mkoani Ruvuma, baada ya wataalam kufika soko kuu la Manispaa ya Songea na kukutana na wafanyabiashara.

Mratibu wa Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria mkoani Ruvuma Wakili George Mollel amesema, Wanaume na Wanawake wote wana haki sawa mbele ya sheria isipokuwa elimu kubwa inaelekezwa kwa Wanawake kwa sababu kundi hilo limekuwa likikandamizwa kwa kiasi kikubwa kutokana na tamaduni na mila zilizopo.

Baadhi ya Wananchi mkoani Ruvuma wamesema licha ya uwepo wa matukio mengi ya ukatili na unyanyasaji kwa Wanawake, pia wapo Wanaume wanaofanyiwa unyanyasaji ndani ya familia zao hivyo wameomba elimu zaidi itolewe kwa Wanaume ili na wao waweze kueleza changamoto wanazokutana nazo ndani ya familia zao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi wilaya ya Songea, Mwanaisha Ndauka amewataka Wananchi wa wilaya hiyo kutonyamazia vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua.