Kinana: Rais hawezi kuuza bandari

0
115

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amezungumzia mjadala wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam huku akiweka wazi kuwa Rais Samia Suluhu Hassan haiwezi kuuza bandari hiyo na kuhoji Rais auze bandari kwa maslahi yapi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mkendo, Musoma Mjini mkoani Mara Kinana alianza kwa kueleza kuwa liko jambo la bandari linazungumzwa na mjadala unaendelea kuwa mrefu.

“Nataka niwahakikishie msiamini kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyekula kiapo eti atafanya jambo ambalo halina maslahi na nchi. Haiwezi kutokea, Rais ambaye tangu amechukua usukani amefanya mambo mengi mazuri, kwa nini aende kuuza bandari, sababu ni ipi?”.,Amehoji Kinana na kuongeza kuwa

“….Serikali imesema tunakwenda kufanya kazi hii kwa nia njema ya kuongeza ufanisi, kuongeza mapato tuweze kufanya shughuli nyngi zaidi za maendeleo. Wamejitokeza watu wameanza kuhoji, wako wanaohoji kwa nia njema ya kujenga ya uzalendo, hatuwezi kusema kila anayehoji anania mbaya.”

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Bara amesema wako wanaotetea mkataba na wametoa ushauri mzuri, na kwamba Serikali ipo tayari kupokea kila ushauri utakaotolewa, kusikiliza hoja na yote hayo yatafanyiwa kazi.

“Kiongozi mzuri ni yule ambaye panapotokea ubishani, watu wanabishana na hoja mbalimbali znatolewa anatulia, anasikikiza.
Anachofanya Rais ni kuwa mtulivu kusikiliza kila hoja kuchambua kila hoja, kutathmini kila hoja, ili muda utakapofika tupate uwekezaji ulio bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” Amesisitiza Kinana.