Usikivu wa Rais Samia unaleta mafanikio makubwa – Kinana

0
142

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahaman Kinana amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili ya uongozi wake yanatokana na utulivu, usikivu, kupokea ushauri na kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya Watanzania.

Kinana ameyasema hayo leo Julai 23, 2023 alipokuwa akihutubia wananchi wa Kondoa mkoani Dodoma katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dk. Ashatu Kijaji kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.

“Kwa hali ilivyo na kwa hatua tuliyopiga tukienda hivi tunavyokwenda mpaka kufika 2025 nina uhakika kila Mtanzania atakuwa na sababu ya kusema tuendelee na CCM, tuendelee na Rais Samia Suluhu Hassan. Hatutokuwa na sababu nyingine yoyote kwanza ni utamaduni wetu Chama Cha Mapinduzi hatubadilishi uongozi katikati ya safari, ukitaka kubadilisha sababu itakuwa nini, hakuna.

Hatusemi haya kwa kujivuna bali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM lakini tunaangalia na wenzetu wa nchi jirani wanakwendaje. Nchi yetu imetulia, ina amani, ina umoja, ina mshikamano, nchi ina malengo, na ina mipango ambayo inatekelezwa na kila mtu ni shahidi, CCM itaendelea kuchaguliwa kwa sababu ina sera nzuri ina ilani nzuri inayotekelezeka,” amesema Kinana.

Aidha, amesema kutokana misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Taifa,  watu waliojaribu kuigawa nchi kwa misingi ya udini wameshindwa.

Kinana atahitimisha ziara yake mkoani Tabora ambapo atapokelewa Julai 29 na Julai 30, 2023 atashiriki mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa na baadae mkutano wa hadhara.