Mjema atembelea TBC, aipongeza kwa mageuzi yaliyofanyika

0
347
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Sophia Mjema akizungumza alipotembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mikocheni, Dar es Salaam.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Sophia Mjema ametembea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam ambapo ametoa pongezi kwa mageuzi makubwa ya kimiundombinu na kimaudhui yaliyofanyika.

Mjema ambaye ametembelea TBC kujionea utendaji kazi amesema mageuzi yaliyofanyika kwenye chombo hicho cha umma yamepanua uwezo wa wananchi kupata taarifa sahihi, na kutimiza wajibu wa chombo cha habari kuwa daraja kati ya wananchi na Serikali.

Akizungumza kuhusu suala la uwekezaji wa bandari katika mahojiano maalum amesema kuwa chama hicho kimeielekeza Serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa uwekezaji huo na namna wananchi watakavyonufaika.

“Tunaendelea kuwaelezea wananchi ili wajue DP World ni nini, ili upotoshaji unaowasumbua wananchi na kuwafanya wawe na hasira na serikali yao wajue sio sahihi,” amesema.

Aidha, akizungumzia suala ya ripoti ya Tume ya Haki Jinai amesema CCM inaunga mkono mapendekezo yaliyotolewa kwa sababu yanagusa maisha ya wananchi kwani ni mambo yanayowakwaza na wanataka kusikilizwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha ametumia nafasi hiyo kumwelezea mikakati ya shirika kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi pamoja na kupanua wigo wa usikivu ili kuwafikia wananchi wote popote pale walipo.