Rais Samia Suluhu Hassan amewakaribisha raia wa Hungary kuja kuwekeza nchini na pia kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo ya ndani na mgeni wake Rais wa Hungary, Katalin Novak, Rais Samia amesema ziara ya rais huyo itachochea watalii zaidi kutembelea Tanzania.
Amesema mwaka 2022 Tanzania imepokea watalii zaidi ya 7,000 kutoka Hungary ambao ni wengi kulinganisha na watalii kutoka taifa hilo waliowahi kuja hapa nchini.
Ameongeza kuwa mara baada ya ziara hiyo, watalii wengi zaidi kutoka Hungary watavutiwa na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania.
Kuhusu elimu, Rais Samia ametoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Hungary kusoma kwenye vyuo vikuu vya hapa nchini na kwa kuanzia wataanza na wanafunzi watano.
Rais Samia pia amezungumzia masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kuweza kufikia malengo ya kuwa na usawa wa kijinsia.