Rais wa Hungary awasili nchini

0
157

Rais Katalin Novak wa Hungary amewasili nchini usiku huu akitokea nchini Rwanda tayari kuanza ziara yake ya kikazi ya siku nne nchini Tanzania kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Rais Katalin amelakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stergomena Tax na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali.

Baada ya kuwasili Rais Katalin amekagua kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichoandaliwa maalum kwa ajili yake na kisha kukagua vikundi mbalimbali vya ngoma za asili na burudani.

Rais huyo wa Hungary Jumanne Julai 18, 2023 anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam kwa mazungumzo ya ndani na kisha kukutana na ujumbe wa pande zote mbili.

baada ya mazungumzo ya ndani, viongozi hao watazungumza na Wananchi kupitia waandishi wa habari kuelezea mambo mbalimbali waliyojadiliana.