TBC ina jukumu kubwa kwa Taifa

0
194

Vyombo vya habari vina jukumu la kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi, vikiiwezesha Serikali kupata maoni ya wananchi, na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya yale ambayo Serikali inatekeleza kwa niaba yao.

Licha ya kuwa jukumu hilo ni kwa vyombo vyote vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema TBC ina jukumu kubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna amani na utulivu nchini.

“Sisi tupo kuwezesha nchi yetu kuendelea kuwa na amani, kuendelea kuenzi utamaduni na kuhakikisha Watanzania wote tunaishi vizuri,” amesema.

Ameweka msisitizo kwenye dhima za TBC katika mahojiano kuhusu ripoti ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliipa TBC jukumu la kuijadili na kuhakikisha wananchi wanaielewa.

Ameongeza kuwa wajibu wa TBC kama chombo cha umma ni kuwa nyenzo ya Serikali iliyoko madarakani kwa kuiunganisha na wananchi walioichagua.