Tume ya Kuboresha Mfumo na Taasisi za Haki JInai nchini imebaini wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kuongozana na Wajumbe wa Kamati za Usalama hata katika ziara ambazo hazistahili kamati hizo kuwepo.
Imesema hatua hiyo ni kuiongezea gharama Serikali kwa matumizi ya magari na posho.
“Wakuu hao kuambatana na Kamati za Usalama katika ziara zao kunasababisha hofu kwa Wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha kero zao kwa kuogopa kukamatwa na pia baadhi ya majukumu yanayopaswa kutekelezwa na Wajumbe wa kamati hizo husimama na pia desturi hii inaiongezea Serikali gharama kutokana na matumizi ya magari na posho.” Imesema Tume
Pia imebaini wakuu wa mikoa na wakuu hao wa wilaya kutumia vibaya madaraka yao ya kutoa amri za kukamata na kuwaweka watu mahabusu na mara nyingi amri hizo hutolewa bila kuzingatia masharti yaliyoanishwa katika sheria, hivyo kutaka jambo hilo likemewe.
Akisoma taarifa rasmi ya Tume hiyo Ikulu, Dar es Salaam mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Tume ya Haki JInai Jaji MKuu Mstaafu Mohamed Othman Chande ameongeza kuwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilava pia wamekuwa wakijitambulisha kama Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kinyume na sheria inayowatambua kama Wenyekiti wa kamati za Usalama za
mikoa na wilaya.