TICTS haikuendana na matarajio ya Serikali

0
138

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali iliamua kusitisha mkataba na kampuni ya TICTS kutoka China iliyokuwa na haki ya kuendesha shughuli za kuhudumia makasha katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na tathmini iliyofanyika kuonesha kampuni hiyo haikuendana na matarajio ya Serikali katika sekta ya bandari.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam.

“Upangishwaji wa TICTS uliendelea kuanzia Serikali ya awamu ya tatu, nne, tano mpaka awamu ya sita. Mwezi Disemba 2022 Serikali ya awamu ya sita baada ya kuona mkataba huu hauendani na matarajio ya Serikali kuhusu maslahi mapana ya nchi yetu iliamua kusitisha mkataba huo”. Amesema Profesa Mbarawa

Aidha, ameongeza kuwa baada ya kusitisha mkataba na kampuni ya TICTS, Serikali ilipokea mapendekezo kutoka kampuni mbalimbali za kuendesha bandari zikiwemo kampuni ya TICTS kutoka China, Port of Singapore Authority kutoka Singapore, DP World kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Abu Dhabi Port kutoka UAE na kampuni zingine kutoka India, Ufaransa na Denmark.