Baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwakamata Wanaume wanaosuka nywele wakiwa Zanzibar bila kibali maalum,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar Dkt. Omar Adam amesema iwapo Mwanaume atakamatwa bila kibali cha kusuka atatakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni moja au kwenda jela kwa kipindi cha miezi sita au kutumikia adhabu zote mbili kwa mara moja.
Akizungumza kwa njia ya simu na TBCOnline Dkt. Omar Adam amesema, watu wamemnukuu vibaya na kwamba sheria hiyo ipo na sio kibali cha shilingi Milioni moja bali ni faini ya shilingi Milioni moja ama jela miezi sita ama vyote kwa pamoja.
Je, Ni nywele za aina gani?
Katibu Mtendaji huyo wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar amesisitiza kusuka aina yoyote ya nywele kwa Mwanaume sio utamaduni wa Zanzibar, hivyo hairuhusiwi na ni kinyume na mila.
“Usuke vitunguu, usuke mbatata, usuke shikamoo Bibi sio utamaduni, wala Rasta sio utamaduni wa Zanzibar”. amesema Dkt.Omar
Kwa wageni?.
Dkt.Omar Adam amesema kwa mujibu wa sheria, sheria haichagui, hiyo sheria inafanya kazi kwa watu wote iwe mgeni iwe mwenyeji na hakuna sheria isiyo na ‘visingizio’.
“Kwa mujibu wa sheria haichagui.. na inavyotakiwa kila mtu anapokwenda kwenye nchi za watu afuate sheria za hao watu lakini chimbuko kubwa la Wazanzibari kusuka nikuona wageni wanasuka lakini hakuna sheria isiyokuwa na ‘excuse’ kwa makundi maalum”. Amesema Dkt.Omar
Neno la Dkt. Omar kwa Vijana
Zanzibar haiwezi kuwa kama Jamaica utamaduni wetu uzingatiwe.
“Vijana wafuate mila na desturi, sheria ipo kulinda mwisho wa siku Zanzibar ibaki Kama Zanzibar na Jamaica Kama Jamaica”.