Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Sunpyo Kim ametembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zilizopo Mikocheni, Dar es salaam kujionea utendaji kazi wa kituo cha Televisheni cha TBC2 ambacho serikali ya Jamhuri ya Korea imefadhili ujenzi wa studio pamoja na vifaa vyake.
Balozi Kim baada ya kukagua utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mradi wa TBC2 amesema amefurahishwa kuona mradi huo ukiwa umetekelezwa kama walivyotarajia, na hivi karibuni watafadhili mradi wa pili wa kituo hicho cha televisheni cha TBC2 ambacho ni mahususi kwa burudani na vijana.
Aidha, Balozi Kim ameipongeza TBC kwa kuwa na vituo maalum ambavyo vinagusa matabaka mbalimbali katika jamii ikiwemo Televisheni ya TBC2 ambayo ni maalumu kwa vijana na burudani, TBC International Radio ambayo inafanya matangazo yake kwa lugha la Kiingereza, Tanzania Safari Channel ambayo ni maalumu kwa ajili ya utalii, taarifa ya habari kwa lugha ya Kiingereza ya TBC News kutoka TBC1 na TBC Online ambayo inatoa habari na matukio kwenye mitandao ya kijamii.