Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Kiula Kingu amefanya ziara katika Kata za Kwembe, King’azi na Msigani ili kuanza utekelezaji wa mpango wa kuboresha huduma za maji safi katika maeneo hayo.
Mpango huo una lengo la kutekeleza miradi miwili itakayotatua changamoto iliyopo ya msukumo mdogo wa maji na ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo.
Awamu ya kwanza itahusisha ulazaji wa bomba kutoka eneo la Kwembe maduka Tisa hadi jirani na Shule ya sekondari ya Barbara Johanson.
Awamu ya pili ya mradi huo itahusisha kazi ya ulazaji wa bomba za inchi 8 kwa umbali wa mita 3,200, mradi ambao ukikamilika utanufaisha wakazi wa Njeteni, Mlimani City, King’azi B, Mzalendo, Kwembe Mpakani, Mama Poa, Maduka Tisa, Mitiki, Kwembe Kijijini, Tawalani na Mwangosi.
Kingu amesema DAWASA tayari ina mabomba na vifaa muhimu vya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo inayotarajiwa kuanza mwisho wa mwezi huu.