Wanafunzi 1,900 waliokatisha masomo warejea shule

0
289

Tangu kutolewa kwa waraka wa kuwaruhusu Wanafunzi waliokatisha masomo mbalimbali kurejea shule, jumla ya wanafunzi 1,907 wamerejea kuendelea na masomo ya sekondari hadi Januari 2023.

Takwimu hizo zimetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga wakati akijibu swali la Tunza Malapo, Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua ni wanafunzi wangapi wamerejea shuleni tangu waraka wa kuwaruhusu utolewe.

Naibu waziri ametoa ufafanuzi zaidi kuwa waliorudi katika mfumo rasmi ni 562 na waliorejea nje ya mfumo rasmi wa elimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ni 1,345.

Aidha, amesema kwa upande wa wanafunzi wa elimu ya msingi wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inaendelea kukusanya taarifa za wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu mbalimbali.