NCAA, Karatu kukabiliana na wanyama hatarishi

0
150

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirkiana na uongozi wa wilaya ya Karatu mkoani Arusha, wamefanya kikao cha ujirani mwema kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kupunguza migogoro kati ya Wananchi na Wanyamapori hatarishi kwa vijiji vinavyozunguka eneo la hifadhi.

Mkuu wa wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba amesema kuwa wamekubaliana na uongozi wa NCAA kuweka mikakati wa kupambana na wanyamapori hatarishi wanaongia kwenye mashamba na makazi ya watu.

Kolimba amesema mikakati hiyo ni pamoja na kujenga uzio wa umeme wa kuzuia wanyama wanaoingia kwenye makazi na mashamba ya Wananchi, kutengeneza mizinga ya nyuki kudhibiti wanyama wakali kama tembo na kutoa elimu kwa jamii ya vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi ya Ngorongoro kujua namna bora ya kujilinda na wanyama wanaovamia maeneo yao.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Elibariki Bajuta amesema kuwa kufanyika kwa kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utalii kukutana na uongozi wa maeneo yanayozunguka hifadhi na kwa pamoja kushirikiana katika kuweka mikakati ya kudhibiti changamoto zinazotokana na wanyamapori waharibifu.