Wabunge wataka ushuru wa mafuta uongoezwe

0
244

Wabunge wameishauri Serikali kuongeza ushuru kwenye mafuta ya kula yanayotoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na ushindani mkubwa kupitia mafuta yanayoingizwa nchini.

Wabunge wametoa pendekeze hilo walipokuwa wakichangia bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24 ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, mwaka huu kiwango cha ushuru kimebaki kama kilivyokuwa mwaka 2022/23.

Awali akichangia bajeti hiyo Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala ameeleza kushangazwa na Serikali kukinzana ambapo wakati Waziri wa Kilimo anahimiza watu kulima alizeti, Waziri wa Fedha na Mipango anapunguza ushuru wa mafuta kutoka nje, hivyo akawataka kuwa na kauli moja ili kutomtatiza mkulima.

Aidha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga naye ameishauri Serikali kuongeza ushuru ili alizeti inayolimwa nchini ikawe salama na ipate soko.

Hata hivyo, akitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri Mwigulu Nchemba amesema kuwa ushuru huo haukuongezwa, lakini wamepokea ushauri wa wabunge kuhusu kuongezwa kwa ushuru huo.

Tuna viwanda 771 vinavyochakata mafuta, tunazalisha tani 300,000 na mahitaji ni tani 560,000, hivyo kupelekea uagizaji mafuta nje ili kuziba nakisi hiyo.