Serikali yaelekeza Watalii kuvua viatu wanapoingia Msikitini

0
409

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Merry Masanja amemuagiza Mkurugenzi wa Malikale wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ashirikiane na viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha Msikiti mkongwe ambao upo wilayani humo unachukuliwa kama misikiti mingine.

Akitoa agizo hilo bungeni jijini Dodoma Masanja amewaagiza viongozi hao kuweka utaratibu utakaowezesha watalii wanaofika kuvua viatu wanapoingia kwenye Msikiti huo.

“Msikiti huu ni sawa na misikiti mingine, na heshima zinazotakiwa kama msikiti, watu waingie bila viatu, basi utekelezaji wake uanze mara moja,” ameagiza Naibu Waziri Masanja

Ametoa maelekezo hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bagamoyo, Muharami Mkenge aliyetaka kujua ni lini msikiti mkongwe utaanza kuhesabika kama misikiti mingine na watalii na watu wengine watakapokwenda wavue viatu wanapoingia ndani ili kutunza mila na utamaduni wa misikiti katika Mji wa Kaole, Bagamoyo.

Kuhusu ukarabati wa majengo ya magofu, Serikali imesema kutokana na umiliki wa majengo mengi kuwa chini ya usimamizi na umiliki wa mamlaka mbalimbali ikiwemo watu na taasisi binafsi, wizara imeendelea kuwahamasisha wadau wote kufanya ukarabati usioathiri mwonekano au kuharibu historia hiyo.

Hadi sasa tayari wadau wanne wamepewa vibali vya kufanya ukarabati wa majengo yao ndani ya Mji Mkongwe wa Bagamoyo.