Wizara ya Fedha na Mipango imesema hadi kufikia Aprili 2023, deni la Serikali lilikuwa shilingi Trilioni 79.1, sawa na ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na shilingi Trilioni 69.4 kwa
kipindi kama hicho mwaka 2022.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2023/24 amesema kati ya kiasi hicho, deni la nje
ni shilingi Trilioni 51.2 na deni la ndani ni shilingi Trilioni 27.9.
Ametaja sababu za ongezeko la deni kuwa ni pamoja na kupokewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya.
Aidha, amesema tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba 2022 imeonesha kuwa deni ni himilivu na viashiria vya deni viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Ripoti ya kampuni za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service kuhusu tathmini ya kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa, Tanzania imewekwa katika daraja la B2 POSITIVE na Kampuni ya Moody’s Investors Service na daraja la B POSITIVE na Kampuni ya Fitch Ratings ambayo yanaashiria taswira chanya kwa nchi kimataifa.