Serikali yaeleza chanzo cha ugonjwa wa Manjano kwa watoto

0
209

Wizara ya Afya imesema kuwa tafiti nyingi zimefanyika kitaifa na kimataifa kujua chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano mara baada ya kuzaliwa na kuonesha kuwa hali ya umanjano ikitokea ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa inaashiria tatizo la kiafya (Pathological) na linahitaji kutambua sababu na kutoa tiba stahiki.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala aliyetaka kujua chanzo cha ugonjwa wa Manjano kwa watoto wachanga.

Akitoa ufafanuzi zaidi Dkt. Mollel amesema tatizo hilo likitokea baada ya saa 24, mara nyingi linatokana na sababu za kawaida za mwili wa mtoto kupunguza chembechembe nyekundu nyingi alizokuwa nazo tumboni kwa mama, hata hivyo amesema uchunguzi wa kina ni muhimu ili kujihakikishia.

Aidha, amesema kwamba tayari Serikali imenunua vifaa maalum kwa ajili ya kuwatibu watoto wenye changamoto hizo ambavyo tayari vimefikishwa kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.