Kizimbani kwa kusababisha hasara ya Mabilioni

0
153

Waliokuwa watumishi wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) pamoja na waliokuwa wafanyakazi wa Benki za NBC na Habib African, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulisababishia shirika la umma hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni mbili.

Watuhimiwa hao wamepandishwa kizimbani na
kusomewa mashitka 48 na Wakili Mwandamizi wa Serikali Hemed Khalid mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mary Mrio.

Wakili wa Hemed amesema washtakiwa hao wametenda makosa hayo katika tarehe tofauti tofauti kati ya Oktoba Mosi, 2011 hadi Machi 01, 2014 ambapo inadawa kwa pamoja walitumia jina ofisi ya Waziri Mkuu kughushi nyaraka pamoja na kiwasilisha nyaraka za uongo kwamba ofisi ya Waziri Mkuu imeidhinisha fedha hizo kupitia benki tofauti kwenda kwa watu tofauti wakati wakijua sio kweli.

Kosa lingine lililotajwa katika hati ya mashtaka ni kuendesha ama kuongoza genge la uhalifu ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo maeneo mbalimbali ndani ya Dar es Salaam kinyume na sheria ili kuweza kujipatia fedha hizo ambazo ni mali ya umma.

Hata hivyo Mahakama haijawaruhusu watuhumiwa hao kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 27, 2023 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamepelekwa rumande.