Wafanyakazi TBC wataka wanaolichafua shirika wachukuliwe hatua

0
184

Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kauli moja wametaka wale wote wanaolichafua shirika hilo kwa kusambaza taarifa na maneno ya uongo wachukuliwe hatua za kisheria.

Wafanyakazi hao wametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wafanyakazi wa TBC uliofanyika katika ofisi za Mikocheni kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya shirika hilo.

Katikati ya mjadala huo Wafanyakazi hao wakaonesha kukerwa na tabia ya watu ambao kwa muda sasa wamekuwa wakisambaza shutuma za uongo dhidi ya TBC, jambo ambalo linahatarisha taswira ya shirika hilo adhimu la umma.

Wakizungumza kwa falsafa za kimageuzi chanya, baadhi ya Wafanyakazi wa TBC wamesisitiza umoja na uchapaji kazi kwa maendeleo ya shirika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Shirika la Utangazaji Tanzania, Felician Maige amesema chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kushughulikia kero za Wafanyakazi kwa uwazii, na mengi yanayosema ni uzushi na uongo wenye nia ya kurudisha nyuma mkakati mkubwa wa maendeleo ya shirika hilo.

Katika mkutano huo Wafanyakazi wa TBC wameipongeza Serikali kwa kutenga fedha zilizoruhusu mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ndani ya shirika hilo.