Haaland, Mchezaji Bora Ligi Kuu England

0
216

Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya England msimu wa 2022/23, ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye ligi hiyo.

Aidha, Haaland mwenye umri wa miaka 22 ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi akiwa ni mchezaji wa kwanza kwenye ligi hiyo kushinda tuzo hizo kwa msimu mmoja.

Haaland amefunga magoli 36 katika michezo 35 na kutoa usaidizi wa magoli nane katika michezo ya ligi aliyocheza.

Tayari ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2023 kutoka Chama cha Waandishi wa Habari wa Soka na pia amepata nafasi katika orodha fupi ya tuzo za Mchezaji Bora wa Msimu wa PFA na Mchezaji Bora Chipukizi wa Msimu wa PFA.

Raia huyo wa Norway ambaye amekuwa na msimu bora amevunja rekodi ya miaka 26 ya kufunga magoli mengi kwenye msimu mmoja wa EPL.

Magoli yake yameiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo EPL, ukiwa ni ubingwa wa tano kati ya misimu sita iliyopita.