Maboresho bandari ya Tanga kuongeza ufanisi

0
157

Bandari ya Tanga imejiwekea lengo la kuongeza uwezo wake wa kuhudumia shehena ya mizigo
kutoka tani Laki 7.5 kwa mwaka za
sasa hadi kufikia tani Milioni Tatu kwa mwaka.

Uwezo huo wa kuhudumia shehena utaongezeka baada ya bandari hiyo ya Tanga kufanya maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza kina cha maji katika eneo la lango la bahari na katika eneo la magati ya kupokelea meli ili kuruhusu meli zenye urefu wa Mita 150 – 200 kutia nanga bandarini hapo.

Akizungumza na waandishi wa Habari bandarini hapo Meneja wa bandari ya Tanga, Masoud Mrisho amesema, mradi wa maboresho ya bandari hiyo umefikia asilimia 99.85 huku asilimia 0.15 iliyobaki ikitarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

Ameongeza kuwa pamoja na kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena, pia gharama za kuhudumia mizigo zitapungua kufuatia maboresho hayo.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Chama cha Wasafirishaji Thorea Halfani ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuifanyia maboresho bandari ya Tanga huku akitoa rai kwa Wadau wengine wa usafirishaji kuitumia bandari hiyo kwani itasaidia kupunguza msongamano katika utoaji wa mizigo.

Mradi wa maboresho katika bandari ya Tanga umegharimu takribani shilingi Bilioni 429.1 na umetekelezwa katika awamu mbili kwa muda wa miaka mitano.