Wasiojulikana waua na kujeruhi Butiama

0
183

Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia nyumba moja wilayani Butiama mkoani Mara na kuua mtu mmoja na kujeruhi mwingine.

Tukio hilo lilitokea Mei 21 katika kijiji cha Nyankanga, ambapo watu hao walivamia nyumba ya Nickson Gisiri na kumuua na kumjeruhi mke wake kwa mapanga.

Inadaiwa kuwa watu hao walivamia nyumba hiyo majira ya saa nane usiku na kutaka Gisiri awapatie shilingi milioni 15, walizodai amepata kutokana na biashara zake za madini.

Mkuu wa wilaya ya Butiama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo Moses Kaegele amesema watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo na uchunguzi unaendelea.

Kaegele amesema baada ya wahalifu hao kukosa pesa waliyokuwa wakiitaka walichukua televisheni na simu na kisha kutokomea kusikojulikana.

Kwa sasa mke wa marehemu anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama na hali yake yake inaelezwa inaendelea vizuri.