Mayele: Azam inakamia sana mechi kubwa

0
323

Mshambuliaji wa Yanga SC, Fiston Mayele amesema mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hautakuwa mwepesi kwa sababu Azam FC ina wachezaji wazuri na huwa wanakamia sana mechi kubwa.

Mayele ambaye amekuwa na msimu bora katika mashindano ya ndani na nje ya nchi ameongeza kuwa namna Azam FC inavyocheza na timu kama Namungo FC ni tofauti sana na ikikutana na Simba SC au Yanga SC.

“Tunajua mechi ya fainali itakuwa mechi ngumu kwa sababu wana wachezaji wazuri, wachezaji wakubwa na wanajua kupania mechi kubwa,” amesema Mayele.

Kuhusu ubora wake kwenye msimu huu, amekiri kuwa huu ni msimu bora sana kwake katika maisha yake ya soka, huku akimuomba Mungu aendelee na kiwango alichonacho sasa hadi mwisho wa msimu.

“Kwangu huu ni msimu bora sana kwa sababu tangu nimeanza mpira kwenye mashindano ya kimataifa sijawahi kufunga magoli sita au saba, nilikuwa naishia tatu, mbili, basi,” amesema Mayele.

Mchezo huo wa fainali utapigwa katika Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.