Dkt Tulia: Posta ongezeni kasi ya huduma kwa Wananchi

0
184

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amelishauri Shirika la Posta nchini kutumia fursa ya uwepo wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Anwani za Makazi kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa Wananchi.

Dkt. Tulia ametoa ushauri huo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, alipotembeqb maonesho ya wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Taasisi zake pamoja na watoa Huduma za habari na mawasiliano.

Miongoni mwa Wabunge waliotembelea maonesho hayo ni Mbunge wa jimbo la Kilosa mkoani Morogoro Profesa Palamagamba Kabudi ambaye amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC).

Ameshauri TBC kupitia chaneli ya Utalii kushirikiana na Kampuni ya Simu Nchini (TTCL) kutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro kupitia mfumo wa mawasiliano uliowekwa katika kilele cha mlima huo.

“TBC imekuwa ni chombo cha habari kinachowafahamisha na kuwaelimisha Watanzania hasa Chaneli ya Tanzania Safari, hii imewafanya watalii wengi wa nje na Watanzania kufahamu utajiri mkubwa wa rasilimali za Tanzania.” Amesema Profesa Kabudi

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tekinolojia ya Habari imeandaa maonesho ya wiki ya wizara hiyo, ambapo taasisi na watoa huduma za mawasiliano na habari zinaonesha huduma mbalimbali zinazolewa.