Waziri Ummy: Suala la vichanga kong’olewa macho ni la ukweli

0
443

Wizara ya Afya imeanza kushughulikia tukio lililotokea mkoani Tabora
ambapo watoto wawili mapacha waliozaliwa kabla ya muda (premature) katika kituo cha afya Kaliua wakiwa hai kufariki dunia saa chache baadaye katika mazingira ya kutatanisha.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema tayari wauguzi waliomhudumia mama wa watoto hao wamesimamishwa kazi.

“Tumelifuatilia suala hili, kuna ukweli. Uongozi wa Wilaya ya Kaliua umeshaanza kuchukua hatua. Baadhi ya Watumishi wa Afya waliomhudumia mama huyu wameshasimamishwa kazi. Nakemea vikali kitendo hiki. Ninamuagiza RMO Tabora kusimamia vyema weledi, maadili na miiko ya watumishi wa afya,” ameandika Waziri Ummy.

Katika madai yake yaliyosambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, baba wa mapacha hao, Kisaka Mtoisenga, mkazi wa Ushikola, Kaliua amesema Mei 09, 2023 saa 4 usiku mke wake alijifungua salama watoto wawili mapacha katika kituo cha afya Kaliua.

Amesema watoto hao walizaliwa njiti na kwa kuwa kituo cha afya Kaliua hakina uwezo wa kuhudumia watoto njiti walipewa rufaa kwenda hospitali teule ya wilaya.

“Kituo hakina gari la wagonjwa, hivyo wakatuambia tukatafute usafiri. Nikamuacha mke wangu na watoto wakiwa wazima wa afya, nikaenda kutafuta usafiri. Muda huo haikua rahisi kupata gari, nikapata Bajaji. Tulipofika wahuhudumu wakasema tusubiri wawaandae watoto,” amesema Kisaka.

Ameongeza kuwa ilipofika saa 5 usiku wahudumu wakawaambia waendelee kusubiri wanaendelea kuwaandaa na ndipo majira ya saa 6 usiku wahudumu wakawaambia bahati mbaya watoto wamefariki na watawapatia maiti asubuhi ya siku inayofuata.

“Asubuhi wakatupatia maiti zikiwa ndani ya maboksi, kwenye chumba maalumu cha upasuaji, ambacho kina giza. Wakatusisitiza tukazike siku hiyohiyo kwa haraka kwa sababu watoto njiti hawafanyiwi msiba. Tulipofika nje kabla ya kupanda gari tukafungua maboksi. Tukakuta watoto wameng’olewa macho, wamekatwa ulimi na wamechunwa ngozi kwenye paji la uso. Tukahamaki. Tukarudi kuuliza nini kimetokea, hawakutupa majibu ya kuridhisha,” ameendelea kueleza baba wa watoto hao.

Amesema wamefuatilia sula hilo Polisi na kwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua ambaye alishauri wakazike.

“Nikataka uchunguzi ufanyike. DC akaagiza maiti zipelekwe hospitali ya Urambo. Hadi leo zipo huko sijui nini kinaendelea. Naomba unipazie sauti Rais asikie. Watoto wangu wametendewa unyama kwenye kituo cha afya, halafu nanyimwa haki kwa kisingizio cha ushirikina? Naumia sana,” Kisaka akihitimisha maelezo yake.