Hospitali ya wilaya ya Karatu yafunguliwa rasmi

0
161

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Leo anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Arusha, yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za Wananchi.

Hapo jana akiwa wilayani Karatu pamoja na mambo mengine, alifungua rasmi hospitali ya wilaya ya Karatu ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 3.37.

Akizungumza mara baada ya kufungua hospitali hiyo Makamu wa Rais amesema, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma bora za afya zinasogezwa karibu na Wananchi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo ya Karatu pamoja na wa hospitali hiyo kusimamia kwa uaminifu dawa zinazolpelekwa na Serikali kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi.

Shughuli nyingine aliyoifanya Makamu wa Rais wilayani Karatu
ni kufungua hoteli ya kisasa ya hadhi ya nyota tano ya Ngorongoro O’ldeani Mountain Lodge, yenye uwekezaji wa shilingi Bilioni 12.

Pia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zinazojengwa katika eneo la Kaminy Estate na
kuwataka Watumishi wa Mamlaka hiyo kuhakikisha wanatambua na kutumia vema dhamana waliopewa ya ulinzi wa rasimali za Taifa zilizopo kwenye eneo hilo.