Maafisa wapya 146 wa JWTZ watunukiwa Kamisheni

0
526

Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 146 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 65/18.

Sherehe hizo za kunutuku Kamisheni kwa Maafisa wa JWTZ, zimefanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson.

Akitoa maelezo ya sherehe hizo Mkuu wa Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) Brigedia Jenerali Stephen Mnkande amesema kuwa Maafisa hao wapya walianza mafunzo Machi 12 mwaka 2018 wakiwa 236 ambapo 94 kati yao wameshindwa kufuzu kutokana na sababu mbalimbali.

Ameongeza kuwa Maafisa 146 waliofuzu wamefundishwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kukubalika kimataifa.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mnkande, Maafisa hao wapya waliotunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu wana viwango mbalimbali vya elimu ambapo Watatu wana Shahada ya Uzamili, 116 wana Shahada ya Kwanza, Watatu wana Shahada ya Juu na 23 ni Madaktari wa binadamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kuiamini, kutoa kipaumbele na kuitumia JWTZ katika majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wananchi na ameahidi kuwa Jeshi hilo litaendelea kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na majukumu ya kijamii.

Akizungumza na Majenerali, Maafisa, Askari na wageni waalikwa, Amiri Jeshi Mkuu Rais Magufuli amewapongeza Maafisa wapya wa JWTZ kwa kufuzu mafunzo yao na pia ameipongeza JWTZ kwa kutekeleza majukumu yake vizuri, kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Rais Magufuli ameelezea kuridhishwa na kazi nzuri za kijamii zilizofanywa na JWTZ zikiwemo za ujenzi wa ukuta katika eneo la madini ya Tanzanite mkoani Manyara kwa miezi mitatu, uamshaji wa kivuko cha MV Nyerere kilichopata ajali katika ziwa Viktoria uliotumia siku Saba, ujenzi wa nyumba 41 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwa muda wa miezi miwili na kukusanya korosho za wakulima katika msimu uliopita.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa JWTZ kupitia shirika lake la Nyumbu kutengeneza magari ya zimamoto kama ambavyo shirikia hilo limewahi kufanya katika miaka ya nyuma, ili nchi iondokane na gharama kubwa zinazotumika kuagiza magari ya zima moto kutoka nje ya nchi.

Ameliahidi Jeshi hilo kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha linajiimarisha katika majukumu yake yote na ametoa wito kwa Maafisa wapya kutambua kuwa wapo katika Jeshi linaloheshimika na hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanaendeleza sifa hiyo njema.