Waziri Mkuu : Akina Baba wasaidieni wake zenu kulea watoto

0
128

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka jamii ishirikiane na akinamama katika malezi ya watoto, ili kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania.

Majaliwa ametoa wito huo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya Mtoko wa Mama, ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani, hafla iliyoandaliwa na taasisi ya Binti Lindi Initiative.

“Akinababa washirikiane na akinamama katika malezi ya watoto, kwani kidole kimoja hakivunji chawa. Sote tumelelewa na akinamama zaidi, lakini akinababa tunapaswa vilevile kujipa muda na kufuatilia mwenendo wa tabia ya mtoto kuanzia asubuhi mpaka usiku”. Amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa jamii kuheshimu na kuthamini mchango wa Mama katika malezi.

“Kama wahenga walivyosema, kuzaa siyo kazi ila kazi ni kulea mwana, tushirikiane na akinamama wote katika malezi ili kwa pamoja tuweze kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania,” amesema Majaliw

Amewataka wazazi na walezi wajitambue kuwa wao ni taasisi muhimu tena ya kwanza katika malezi ya mtoto.

Siku ya Mama Duniani huadhimishwa Jumapili ya pili ya mwezi Mei kila mwaka.