Scott Morrison Waziri Mkuu mpya Australia

0
2545

Chama cha Liberal nchini Australia kimemteua Scott Morrison kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo kuchukua nafasi ya Malcolm Turnbull ambaye ameondolewa kwa lazima na chama chake.

Kutokana na mzozo wa uongozi ndani ya chama cha Liberal, viongozi wa chama hicho waliamua kuitisha uchaguzi na kumchagua Morrison ambaye ni Mweka hazina wa chama hicho kwa kura 45 huku mpinzani wake Peter Dutton akipata kura 40.

Morrison anakuwa Waziri Mkuu wa 30 wa Australia, nchi ambayo imeendelea kushuhudia mgogoro wa uongozi ndani ya kipindi cha miaka 10.

Turnbull mwenyewe hakuwania tena nafasi hiyo na mara nyingi amekua akipuuzia wito wa kumtaka ajiuzulu kutokana na mgogoro huo wa uongozi ndani ya chama cha Liberal, mgogoro unaoelezwa kuwa unadhoofisha hata utendaji kazi wa serikali.