Onyango aandika barua kuomba kuondoka Simba

0
865

Beki wa Simba SC, Joash Onyango ameandika barua kuuomba uongozi wa klabu hiyo kuvunja mkataba wake uliobaki ili aweze kwenda kutafuta maisha ya soka nje ya miamba hiyo ya Msimbazi.

Mkataba wa Onyango ambaye alijiunga na Simba Agosti 2020 akitokea Gor Mahia ya Kenya unatarajiwa kumalizika msimu ujao, ambapo aliongeza mkataba wa mwaka mmoja baada ya mkataba wa awali kumalizika.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilizonukuliwa na gazeti la Mwananchi zinaeleza kuwa chanzo cha kutaka kuvunja mkataba ni lawama anazopokea kila anapofanya kosa kwenye michezo mbalimbali.

“Tunaweza tusiwe naye msimu ujao kwa sababu hata viongozi walikuwa wanamtafuta sababu ili kumwondoa kikosini, hivyo kwa sababu yeye mwenyewe kaomba kuondoka msimu ukiisha utaratibu utafanyika,” kimeeleza chanzo hicho.

Hata hivyo, raia huyo wa Kenya amesema hawezi kuzungumzia suala hilo, na kwamba watu sahihi wa kuulizwa ni viongozi.